SOMO






JE AHADI ZA MUNGU NI HALISI KATIKA MAISHA YAKO?

Tuombe!

Wewe Roho mtakatifu nakushukuru kwa ushirika wako wa ajabu kwetu, hata umetupa wakati huu kujifunza neno la Mungu wetu, ahsante sana. Tunakuomba Roho Mtakatifu fungua macho yetu ya ndani ili tuone kile Bwana anataka tuone, tusikie kila Bwana anataka tusikie, zaidi ya yote tupe uwezo wa kuliweka katika matendo somo hili. Tunakushuru Mungu kwa pendo lako maana ndio lililofanya Roho Mtakatifu atuhudumie sasa. Ahsante Yesu kristo kwa neema yako ambayo inatupa kustahilishwa pale tusipoweza, tuwezeshe sasa kuzijua siri za Mungu katika jina la Mungu Baba, mwana na Roho Mtakatifu amen!


UTANGULIZI

Ahadi ni ushawishi ambao upande mmoja hushawishi upande wa pili ili ule upande wa pili ukaubaliane na kile ambacho upande wa kwanza unakiona ni bora. Au Ahadi ni mapendekezo au usihi unaotolewa na upande mmoja kuusihi na kupendekeza jambo fulani ili upande wa pili ukubaliane nao.

Ili ahadi iwe na ahadi lazima kuwepo na pande mbili, upande unaoshawishi, sihi,pendekeza jambo na upande unaokubali ushawishi huo, mapendekezo hayo na usihi huo. Na ule upande wa kwanza uliotoa ahadi lazima uwe na uwezo na nguvu ya kutekeleza yale ulioahidi. Upande wa kwanza pamoja na kushawishi au kutoa mapendekezo pia huwa na masharti au vigezo vya kufuatwa na upande wa pili. Upande wa pili hauwezi kuikubali ahadi ni mpaka pale umeridhika na kukubaliana na masharti na vigezo vya hiyo ahadi. Upande wa pili una kazi moja tu ya kukubali ahadi au kuikataa, lakini hauna nafasi ya kurekebisha masharti ya ahadi.

Mfano: michezo inayoondeshwa na makampuni yanayozalisha vinywaji venye visibo hupenda kutoa zawadi ambazo zimewekwa ndani ya kizibo. Hii ni ahadi ambayo kampuni inakushawishi wewe unywe kinywaji chao, kampuni hutoa masharti fulani kwamba pamoja na kunywa kinywaji chao na ukipata zawadi lakini lazima masharti fulani yazingatiwe, yaweza wakatoa sharti kuwa hicho kizibo kipeleke ofisi zao. Sasa kama wewe utapata kizibo chenye zawadi na usipokipeleka katika ofisi zao haina maana kuwa wewe ni mshindi, ushindi wako utakamilika tu ukipeleka kizibo. Pia kunywa kinywaji chao haitakuwa na maana kuwa umekubaliana na ahadi yao na kuwa umeingia kwenye mchezo wao. Hivyo kila ahadi ina masharti na vigezo vyake.

Sasa basi, Ikiwa upande wa kwanza umetoa ahadi na upande wa pili ukaikubali hiyo ahadi, basi pande hizo mbili hufungamana na hiyo ahadi hugeuka na kuitwa mkataba au agano. Na pale utakapokuwa Mkataba au agano basi kila upande utakuwa na wajibu wake wa kutekeleza. Pale uanapokuwa ni mkataba basi hakuna uchaguzi kwa upande wowote lazima ubanwe na masharti ya mkataba husika. Na kila anayekiuka masharti basi kuna madhara au adhabu htuolewa kwa aliyekiuka.

Turudi kwenye biblia, kitabu cha biblia ni neno la Mungu, Mungu ndo anaongea na kutoa ahadi zake kwa wanadamu, Mungu ndo anamshawishi mwanadamu akubaliane na masharti na vigezo anavyoviweka. Mungu hamlazimishi mtu kukubali ameweka uhuru wa kuchagua ukubali au ukatae hiyo ahadi. Unapoikubali ahadi ina maana unafanya agano na Mungu. Hebu tusome wote

  Kutoka 19:5

Sasa basi ikiwa mtaiitii sauti yangu kweli kweli na kulishika agano langu hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu maana dunia yote pia ni mali yangu

Mungu anawaahidi wana wa Israel kuwa yeye Mungu atawafanya tunu, ahadi ya Mungu ni Israeli wawe tunu. Ila anaendelea kutoa masharti na vigezo ambayo Israel wanatakiwa kufuata ili wawe tunu. Masharti na vigezo hivyo ni-

·         Israeli waitii sauti yake kweli kweli,

·         Israel walishike agano lake  

Kwa hiyo ni juu ya Israel kuchagua kuitii sauti na pia kufuata agano au kutokutii, endapo Israel watatii sauti na wakishaingia kwenye agano na wakilishika hilo agano basi Israeli wawe na uhakika kuwa watakuwa Tunu kati ya makabila yote.

Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake, na hutimiza upande wake. Na analithibitisha hili kwa kinywa chake mwenyewe, sikia asemavyo

v   Zaburi 138:2c

“…Kwa maana umeikuza ahadi yako kuliko jina lako lote”

“…Ahadi yako ni kuu kuliko jina lako” (biblia habari njema Tafsiri ya ushirikiano wa makanisa)

Ina maana ahadi aliyoitoa anaiheshimu na kuikuuza kuliko hata alikuzavyo jina lake. Anasema yeye si mwongo anachokiahidi anatenda.

v  Isaya 46;11b

Naam nimenena nami nitatekeleza, nimekusudia nami nitafanya

 

v  Zaburi 89:34

mimi sitalihalifu agano langu sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu

Hii ni baadhi tu ya mistari ambayo Mungu anakuthibitishia kuwa yeye si muongo kwamba kila ahadi lazima aitimize. Sasa kama ahadi hazitimii tatizo si Mungu bali ni wewe.

 

KWANINI “TUNAONA” AHADI ZA MUNGU HAZITIMII

Pamoja na mistari ambayo Mungu mwenyewe anatuhakikishia kuwa kila ahadi yake ataitimiza na wala hasemi uongo. Watu wengi wamekata tamaa na kuona neno la Mungu ni gumu, ni kama ndoto haliwezi kutimia au neno hilo ni la watu Fulani, au unaona Mungu anachelewa. Mungu hachelewi wala hawai yeye anatenda kwa majira na wakati wake. Na Mungu ni mwaminifu na ameikuza ahadi yake kuliko jina lake mwenyewe.

 Hizi ni baadhi tu ya sababu ambazo zinapelekea watu waone ahadi za Mungu hazitii-

i). KUTOFUATA MASHARTI NA VIGEZO VYA AHADI HUSIKA.

Ni kweli Mungu wetu ni wa neema sana, ni mpole na mwenye huruma nyingi. Lakini hii haifanyi akiuke utaratibu, masharti na vigezo alivyojiwekea kwenye ahadi husika. Kumbuka kila ahadi ina vigezo na masharti husika. Wewe ndo unatakiwa ukubaliane na hayo masharti na vigezo, ukishakubali unakuwa umeingia kwenye agano au makataba. Wengi wa wakristo hajawahi ingia kwenye agano na Mungu, yaani hajawahi kukubali vigezo na masharti ya agano husika. Wamejikuta wameng’ang’ania na kusubiria matokeo ya ahadi huku hawako ndani ya mktaba/agano.

Wakristo wengi huwa wanachagua baadhi ya mistari katika biblia na wanachagua matunda tu ya huo mstari wala hawafuatilii masharti na vigezo vilivyopo katika mstari husika. Wakishachagua hayo maneno basi hubaki wakiyaombea na kumkumbusha Mungu wakati hawajakidhi masharti na vigezo husika. Hebu tuangalia baadhi ya ahadi ambayo wakristo wengi wanaipenda na wameikariri lakini

v  Kumbukumbu 28:1-14

1-“ikiwa utakaposikia sauti ya BWANA Mungu wako, kwa bidii, kutunza kufanya maagizo yake nikuagizayo leo ndipo……”

3- “utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani, utabarikiwa uzao wa tumbo lako…”

Ukiangalia hii ahadi ya kubarikiwa imeanza na masharti na vigezo ambayo ni

·         Kusikia sauti ya Bwana Mungu,

·         kwa bidii,

·         Kutunza kufanya maagizo yake.

 

Kusikia na kusikiliza ni vitu viwili tofauti.

 Kusikikiliza ni kitendo cha kutegea sikio sauti Fulani waweza kuuelewa huo ujumbe au usiuelewe, na kama umeuelewa huuchukulii hatua ya kimatendo kuufanyia kazi.

Lakini kusikia ni kutegea sikio kwa makini jambo Fulani,kisha unalitafakari na kulielewa baadae unachukua hatua za kimatendo kufanyia kazi ujumbe huo. Kusikia ni sawa na kutii, yaani kufanyia kazi ulichoambiwa.

 

Wakristo wengi wanasikiliza neno na ahadi za Mungu, wala hawazikii. Katika huo mstari wa kwanza wa kumbukumbu Mungu anataka usikie akuagizayo yaani utii, tena sio kutii tu bali kutii kwa bidii. Kwa maana hiyo Mungu anataka utii maagizo yake na utii kwa bidii na ndipo hapo atakapokubariki mjini na mashambani.

Mungu haishii kukwambia utii ila anataka pia uyatunze hayo maagizo. Kutunza huku sio kwa kukariri, anamaanisha uweke ndani ya moyo wako , usisahau maagizo yake muda wowote,mahali popote na nyakati zozote maagizo yake uyakumbuke na uyatende.

Usiwe ni mkristo wa kutii sauti ya Mungu ukiwa katika mzingira Fulani tu, au kwa muda Fulani tu. Mungu anataka muda wote na mazingira yote umtii hapo ndipo Baraka zake zitakufuata. Ukisoma vizuri hii mistari ya kumbukumbu huoni mahali Mungu anasema uombe juu ya hizi Baraka. Ina maana ukifuata masharti na vigezo Baraka zitakufuata tu, hutasumbuka kuziomba. Na utakapofuata hayo masharti na vigezo ina maana utakuwa umeingia kwenye agano na Mungu na Mungu naye atakutazama tofauti na amtazamavyo ambaye yuko nje aya agano.

Hebu tuangalie mfano wa baba yetu Ibrahimu ambaye alijikuta ana maagano na Mungu.

v  Mwanzo 12:1-9

Mungu anamwagiza Abram atoke katika nchi yake, mpaka pale Bwana atakapomwonyesha. Mungu anampa ahadi Abramu kuwa atamfanya taifa kubwa na atambariki kila ambarikie na kumlaani kila amlaanie. Pamoja na kumuahidi ahadi ya taifa kubwa na ulinzi wa kipekee bado Mungu anampa sharti Abramu atoke toka katika nchi yake.

Pata picha ni wewe umeshajijenga, una mji mkubwa, mali, una majirani wazuri, ardhi nzuri na umeishi miaka yote hapo, ghafla leo unaambiwa ondoka na unapoendea hupajui na hujapata taarifa zake na hujui utasafiri kwa muda gani mpaka huko. Si rahisi kukubali kuondoka lazima utaanza kufunga na kuomba ili kumuuliza Mungu au kuijaribu hiyo sauti kama ni ya Mungu au laa, na wakati mwingine waweza hata kumbembeleza Mungu akuepushe na hiyo sauti. Lakini kwa kuwa ilikuwa ni ahadi ya Mungu kwa Abramu na hayo ndo masharti yake ya kufanywa awe taifa kubwa na apewe ulinzi wa kipekee alitii. Na Mungu hakumbariki alipoanza safari, na wala hakumsemesha njiani mpaka alipofika ndipo Mungu anamwambia hapo ndipo. Na ukisoma mwanzo 13:2 inasema Abramu alikuwa tajiri. Utajiri wa Abramu ulikuja baada ya kutii ile kutoka tu pale hali yake ya uchumi ikabadilika. Maana sura ya 12 haisemi kuwa alikuwa tajiri.

Kila usomapo neno la Mungu tafuta kwa undani zaidi kama wana wa Beroya waliochunguza maandiko (mdo17:11) kujua masharti na vigezo unavyotakiwa wewe kuvifuata, na uwe na bidii kuvifanya. Kuna baadhi ya mistari huwezi kuona masharti na vigezo moja kwa moja ni mpaka uende mstari mwingine, hebu tuangalie mfano huu

v  Kumbukumbu 28:7

Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako, watakutokea kwa njia moja lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba”

Huu mstari ni mwendelezo wa Baraka na ahadi za Mungu kwa wale tu watakao sikia sauti yake na kutunza maagizo yake. Kwa mstari huu wa 7, lazima utafute maagizo yake ni nini kuhusu adui wainukao juu yako. Ni rahisi kuanza kuwalaani adui zako na kuowaombea wafe, je ndivyo Mungu asemavyo juu ya adui zako, aliposema watakimbia kwa njia saba ina maana unatakiwa uombe wakimbie? Mstari huu lazima usomwe na

v  Rumi 12:19

“wapenzi msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa kisasi ni juu yangu mimi….”

Je kwa mstari huu inapaswa tumkumbushe Mungu ataulipizie visasi? Maana yeye ndo mwenye uwezo na mamlaka ya kutulipia visasi. Bado tunahitaji kuchunguza maandiko mengine juu ya adui zetu. Soma huu

v  Mathayo 5:43-44

“mmesikia kwamba imenenwa umpende jirani yako na umchukie adui yako lakini mimi nawaambia wapendeni adui zenu, waombeeni wanao waudhi”

Yesu anataka tuwapende adui zetu na tuwaombee. Sasa ili adui zako waliokuja kwa njia moja watoke kwa njia saba huna budi kuwapenda na kuwaombea. Hiyo ndio kazi yako. Harafu suala la visasi na ghadhabu na kuwafukuza si lako ni la Mungu. Kwa hiyo kwa mstari wa 7 wa kumbukumbu sharti na kigezo chake ni kumpenda adui yako na kumwombea, jinsi ya huyo adui kutoka si lako ni la Mungu. Na kumwombea adui haina maana uombe atoke, ina maana uombe mema yamkute si mabaya maana umpendaye huwezi kumwombea apatwe na mabaya.

Hii ni mifano michache tu itakayokufanya uweze kuzichunguza ahadi za Mungu na kuzifuatilia kwa bidii na kuyatenda masharti yake. Usijaribu kumlazimisha Mungu atimize Ahadi yake kwako wakati wewe hujaingia kwenye agano naye, yaani hufuati masharti na vigezo vya kila ahadi.

ii. KUTAKA NJIA ZA MKATO

Wakristo wengi wanataka njia ya mkato ili Mungu atimize ahadi yake. Wengi wanataka waombewe au waombe wanyewe kwa muda mrefu na kwa kufunga sana wakidhani Mungu ndipo atatimiza ahadi yake, sahau, Mungu ni Mungu wa taratibu na kanuni fuata masharti naye atatimiza. Sina maana usiwe ni mtu wa maombi la hasha, fanya maombi ila jiulize unakidhi masharti na vigezo vya hiyo ahadi uitakayo. Hebu tazama mfano huu

v  Mathayo 20:20-23

Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambaia, wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wa kuume na mmoja mkono wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akesema hamjui mnaloliomba…lakini kukutei mkono wangu wa kuume na mkono wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na baba yangu”

Ina maana huyu mama alipenda sana wanae waketi katika ufalme wa Yesu. Alitumia njia ya mkato kwa kuomba kuwa Yesu aamuru hivyo. Naye Yesu anamwambia wazi hujui uliombalo maana Yesu alikwisha wafundisha kuwa kwenda kwa baba ni kujikana na kuubeba msalaba wake mwenyewe, badala ya kuomba nguvu na uwezo wapewe wanae ili waweze kila mmoja kujikana na kubebe msalaba wake yeye anataka njia ya mkato.

Ndivyo wakristo wengi walivyo hawana tofauti na mama huyu, hawataki kutii maagizo ila wanapenda njia za mkato. Tusidanganyike Mungu wa Israel hatendi nje ya kanuni zake.

 

KUNA WAKATI MUNGU HAJIBU MAOMBI YAKO BALI ANATIMIZA AHADI YAKE.

Ukiwa na bidii ya kusikia na kutunza maagizo ya Mungu, kuna mambo Mungu atakutendea ambayo hajatokana na maombi yako bali kwa utii wako Mungu anakutendea tu.

v  Kutoka 6:4-5

“tena nimelithibitisha agano langu nao kuwapa nchi ya Kaanan nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni. Na zaidi ya hayo nimesikia kuugua kwao wana wa Israel, ambao wamisri wanawatumikisha nami nimelikumbuka agano langu…”

Pamoja na wana wa Israeli kuomba na kuugua kwa ajili ya mateso waliyoyapata toka kwa Wamisri lakini Mungu hakuwajibu maombi yao, maombi ya Wa Israeli yalimkumbusha Mungu ahadi yake kwa Ibrahimu. Mungu hakujibu maombi yao alichofanya ni kutimiza ahadi yake na agano aliloingia na Ibrahimu. Maana alimwahidi Abramu kuwa atakuwa na uzao mkubwa na huo uzao utakaa ugenini miaka 400, (mwanzo 15:14) Abramu alitenda upande wake alikuwa ameshafariki, uzao wake unaenda ugenini wakati Abramu ameshatimiza masharti ya agano, lilibaki la miaka 400 ugenini. Na ndio maana Israel wakajikuta wanaendelea kuzaliana Misri na hakuna anayekumbuka kurudi kaanani, mpaka miaka 400 ilipotimia ndipo Israeli wanashtuka na kuunza kuugua na kumlilia Mungu. Mungu naye hawatoi Misri eti kwa kuwa wameomba sana au wameugua sana, Hapana! Anawatoa tu kwasababu amekumbuka alichoagana na Abramu. Kutoka kwa wana wa Israeli Misri ilikuwa sio maombi, walitoka sababu ya agano la Mungu na Abramu.

Ukiingia kwenye agano na Mungu uwe na uhakika hilo agano husika Mungu atalilinda vizazai hata elfu, wewe utapita lakini uzao wako utalindwa kwa mujibu wa agano uliloingia na Mungu wako. Maana ndivyo asemavyo

v  Zaburi 105:7-8

“Yeye Bwana ndiye Mungu wetu duniani mwote mna hukumu zake, analikumbuka agano lake milele, neno lile aliloviamuru vizazi elfu”

Unachopaswa ni wewe kung’ang’ania kufuata maagizo yake tena kwa bidii ukiwa bado u hai, na Mungu hatakuacha wewe wala uzao wako. Maana Ibrahimu alikufa akiwa ameacha watoto wanane tu, lakini leo hii ni taifa kubwa sana ambalo Mungu bado analilinda kama mboni ya jicho lake. Japo Israeli wanamuudhi na kumtenda dhambi, lakini ile mbegu aliyopanda Ibrahimu ya utiifu wa maagizo ya Mungu ndio inayoifanya Israeli ya leo iwe taifa teule mbele za Mungu. Yote hii n agano la Mungu na Ibrahimu.

Hebu angalia maisha ya sasa ya wakristo, sio wakristo kwa majina, hapana naamnisha watu waliojikana na kukubali kumfuata Yesu Kristo maana hao ndio wakristo, angalia maisha yao ya kiuchumi ni duni au dhaifu hawako katika kile kiwango ambacho Mungu anataka wawe.wengi wao wanajua kabisa masharti ya agano la uchumi kumtolea Mungu zaka, sadaka, dhabihu na matoleo mengine. Lakini wao ni wachungu na wachoyo mno kutoa, wamejionea huruma kiasi cha kushindwa kumtolea Mungu.

v  Malaki 3:10

“leteni zaka kamili ghalani, …. Asema BWANA wa majeshi, mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagia baraka hata isiwepo nafasi ya kutosha au la”

Huu ni mstari mmoja tu kati ya mingi uhusuyo uchumi, na Mungu anataka zaka kamili sio nusu nusu. Sitapenda kwenda huku zaidi maana si somo husika. Ila nilitaka ujue kuwa kila ahadi inapaswa kushughulikiwa kivyake na sio kuchanganya.

Mkristo

KUMBUKA

Kwenye biblia kuna ahadi nyingi sana za Mungu na kila ahadi ina masharti na vigezo vyake, na huwezi kutumia kigezo na sharti la ahadi Fulani katika ahadi ingine. Kila ahadi inajitegemea.

Maandiko yote nimetoa katika Biblia Maandiko Matakatifu, kinyume cha hapo imeelezewa wapi yametolewa pembeni mwa kifungu husika.

Waweza kuuliza swali kupitia

njiazamungu@gmail.com

0719687343 (meseji tu)

Au sehemu hii chini ya coments

Karibu.

 



SIFA ZAWEZA KUKUTENGA NA MUNGU      
Tuombe,
Ninakushukuru Mungu baba kwa neema yako uliyoiachia kwa ajili ya msomaji huyu, Yesu ninakuomba umlinde msomaji huyu anaposoma na atakapomaliza na siku zake zote, zaidi ya yote Linda neno hili ndani yake lisimtoke likafanyike Mbegu  ndani yake yenye kumzalia Mungu matunda mema, Roho Mtakatifu mfundishe kwa lugha na uweza wa pekee na umuwezeshe kuliweka somo hili katika matendo. Ninakuomba eeh! Mungu baba katika jina la Yesu Amen!
SIFA

Ni hali, namna ambayo ua maneno yanayomuelezea mtu namna gani yuko au kitu Fulani namna kilivyo. Wakati mwingine yaweza ikawa ni aina ya vitu unavyomiliki vikakuelezea jinsi ulivyo, kwa vitu hivyo tunapata sifa za mtu Fulani.
Yaweza ikawa sifa mbaya au nzuri machoni pa watu wengine hata mbele za Mungu, lakini katika somo hili nitazungumzia sifa nzuri mbele za watu hata mbele za Mungu. Yaani sifa hizi zaweza kukutenga na Mungu. Hujakosea kusoma ni kweli sifa nzuri zaweza kukutenga na Mungu.

  
Mfano wa sifa ninazotaka tusome leo:
i.                     yawezekana unamiliki mali nyingi zote umepata kihalali na kwa uwezo wa Mungu wa Israel
ii.                   yawezakana ukawa na cheo kizuri na umepata kihalali.
iii.                  Yawezekana ukawa na huduma nzuri tena inayoongozwa na Mungu.
iv.                 Yawezekana ukawa mume/mke mzuri katika ndoa.
v.                   Yawezekana ukawa na watoto wenye nidhamu na mwenendo bora katika jamii.
Na mengineyo yanayofanana na hayo ambayo yote yamekuja kwa msaada na nguvu za Yesu na ni halali kabisa.
KUMBUKA:
·         yakobo 1:13-14 inasema
mtu ajaribiwapo asisema ninajaribiwa na Mungu;maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakina kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa

yakobo ana maana kuwa mtu anashawishiwa na tamaa zake mwenyewe na kudanganywa. Mtu hudanganywa na shetani. Na shetani hakudanganyi au hakushawishi kwa kitu ambacho huna au huna haja nacho au hukihitaji. shetani anatumia vitu ,nafasi,hali uliyonayo ili akushawishi na kukudanganya.

NAMNA AMBAVYO SHETANI HUTUMIA SIFA ZAKO KUKUDANGANYA

i.                    hukuletea roho ya kujiinua na kutomtii Mungu/roho ya kiburi
mfano , lusifa mwenyewe alikuwa kerubi mzuri mkuu wa ibada za sifa huko mbinguni, kwa sababu ya ustadi wake na cheo chake cha ukuu wa sifa akajiinua hata akajiona yuko sawa na Mungu. Hivyo ndani ya sifa kuna urahisi wa wewe kudanganyika na shetani.

o   Ezekiel 28:1-8
Ni habari za mfalme wa Tiro ambaye alikuwa na mali na hekima kuu, mali hizi alizipata toka kwa wa Israel ambao walikuwa watumwa wake, baada ya Israel kuasi wakawa utumwani kwa mfalme wa Tiro.kutokana na mali hizo mfalme wa Tiro alithubutu kujiinua na kusema yeye ni Mungu na ameketi kwenye kiti cha Mungu.
Mali za mfalme wa tiro zikampa kiburi hata akasahau kuwa hizo mali alizipata toka kwa Mungu wa Israel, maana hasira za Mungu zilipowaka juu ya Israel kwa kosa la kuabudu miungu, Mungu mwenyewe akawauza kwa wa Tiro, mali za Israel zikawa za Tiro, ujuzi, taaluma na ufundi wote wa Israel ukatumiwa wa Tiro hata Tiro ikawa tajiri kuliko Israel. Baada ya utajiri huo mfalme akapata sifa nyingi hata kwa mataifa mengine, moyo na akili yake ikajaa kiburi hakuona umuhimu wa Mungu tena.

Umewahi kujiuliza swali, kwanini wakristo wengi wanapoinuliwa kichumi utiifu wao kwa Mungu unapungua? Au wengine kupote kabisa?
Kinachowapoteza sio mali ni sifa zilizotokana na hiyo mali. Mungu alijua hayo akawatahadharisha wana wa Israel watakapopata mali nyingi wasije kumuacha(kumb 8:18-19). Kuwa na mali nyingi si tatizo wala dhambi ila shateni hutumia hiyo ili akushawishi (yakobo 1:13-14) na upande kiburi kama mfalme wa Tiro kisha umuache Mungu.

Kiburi hakiji kwenye mali tu, hata kupitia elimu, kwanini wasomi wengi wako mbali na Mungu? Ni sifa ndo zimewapumbaza hata wameanza kutumia ujuzi wao kumchimba Mungu kama vile wafanyavyo katika masomo yao, shetani anatumia elimu yao na kuwajaza kiburi ili wamchunguze Mungu na njia zake kwa kumlinganisha na elimu zao.

Umewahi kujiuliza kwanini watumishi wanatumia muda mwingi madhabahuni kusema watumishi wenzao? Kuna mahali kwenye maandiko Mungu amempa mtumishi yoyote kibali cha kukagua kazi ya mtumishi mwenzie?kila mtumishi ana ngwe(plot) yake shambani mwa Mungu, kama kila ngwe iko tofauti na nyenzie unawezaje kuisemea ya mwenzio na nani iasemee yako? Haya yote huja sababu ya ushawishi wa shetani kupitia ile jinsi na namna ambayo Mungu amemwinua huyo mtumishi, sasa shetani anaanza kumpoteza uelekeo kwa kupitia Baraka hizo hizo za Mungu,anamletea kiburi kujiona ni bora kuliko wengine.

Chunga sana roho yako kwa kila hatua ya kubarikiwa kwako kimaisha na kiroho usimpe ibilisi nafasi akakujaza kiburi.

ii.                  Kutokumtegemea tena Mungu katika mambo yako.
o   1nyakati 21:1-
mstari wa kwanza unasema “Tena shetani akasimama juu ya Israel akamshawishi Daudi kuwahesabu Israel…” ( msisitizo nimeuongeza)

toka Daudi awe mfalme wa Israel hakuwahi kushindwa vita, kila vita alivyopigana alishinda, hivyo Daudi alikuwa na sifa ya kuwa mpiganaji mzuri wa vita, na kila vita Daudi hakuenda kupigana pasipo kumuuliza Mungu kama aende vitani au la,na kama akienda atashinda vita au atashindwa . Hivyo Daudi alipigana vita kwa uweza wa Mungu.
Shetani naye akatumia sifa hiyo ya kushinda vita hata akamshawishi Daudi ahesabu watu wake ili ajue idadi ya askari wake. Kitendo cha Daudi kutaka kujua idadi ya askari wake ina maana Daudi alijiona kuwa kwa uwingi wa askari basi atashinda vita na sio tena kwa uweza wa Mungu.
Hivyo Daudi alianza kujitegemea na si kumtegemea tena Mungu.

Angalia mfano wa Yesu katika kitabu cha Luka 12:16-20 juu Yule tajiri ambaye shamba lake lilizaa matunda mengi sana hata akakosa pa kuhifadhi,huyu tajiri aliumua abomoe ghala zake zote kisha ajenge mpya ili ajaze mavuno yake, na lengo la kujenga ghala mpya ni kuhifadhi mavuno yake mpaka pale atakapokufa na ili apate muda wa kutosha kustarehe na wenzie. Mungu akamkemea huyo tajiri kuwa ni mpumbavu hajui uhai wake uko kwa Mungu.
Bila shaka huyu tajiri alitumia nguvu kulima shamba lake, na alipovuna ule wingi wa matunda ukampa sifa ambayo ikamfanya aone kuwa uhai wake uko katika mavuno, akategemea matunda yake kuwa ndo yatampa siku nyingi za kuishi dunian pia yatamfanya astarehe na kuwa na amani. Alitegemea mavuno kuleta uhai na amani. Hapa Mungu aliwekwa kando kabisa.

Ndivyo ilivyo kwa watu wasasa wanapobarikiwa akili zao na mioyo yao inahamia kwenye hizo Baraka, wanaanza kuzitegemea hizo Baraka badala ya Mungu. Angalia kijana kabla ya kuingi katika ndoa nakuwa na uhusiano mzuri na Mungu, na humshirikisha Mungu katika kupata mwenzi. Ghafla akipewa mwenzi basi hutumia akili zake kuendesha ndoa.

Angalia fukara humshirikisha Mungu katika kila jambo, ghafla apatapo mali, huacha kumshirikisha Mungu, na kama atamshirikisha ni katika baadhi ya mambo lakini si yote. Anaanza kutegemea mali zake kutatua matatizo yake na sio Mungu tena.


iii.                Dharau.
*Ezekiel 26:2-
ni habari za Mfalme wa Tiro ambaye kwa utajiri wake alianza kuikebehi na kudharau Yerusalem mji wa Mungu, dharau zilimjaa mfalme wa Tiro.

Naamini wewe ni shahidi mzuri wa maisha yako na jirani zako, kumbuka wakati hujabarikiwa kila jirani ulimuona mzuri na ukashirikiana nae, ulitii agizo la Yesu mpende jirani yako kama nafsi yako. Nini kimetokea baada ya kubarikiwa? Mungu kabadlisha maagizo yake? Amekuaguza uchague huduma za kumpa jirani yako? Au ubague jirani zako.

Kabla ya kubarikiwa ulikuwa na uhusiano mzuri na watumishi wa Mungu baada ya kubarikiwa, unawona watumishi wa Mungu ni njaa tupu wanashida ya hela zako, hata wanapokutafuta unataka waweke kwanza miada(appointment),mbona zamani uliposikia mtumishi kaja kukutembelea tena bila miada ulimsikiliza.

Kumbuka kabla hujawa na cheo ulikuwa unaweza kumchezea Mungu kwa pambio hata kupiga makofi ya nguvu,leo hii unapiga makofi madogo hata mbu akikatisha kwenye viganja vyako wakati wa kupiga makofi hawezi kufa kwa kofi lako,je Mungu kabadilika namna ya kumsifu? Au zamani ilikuwaje? Dharau! Unamdharau Mungu japo hujui kama unamdharau.

Jichunguze umepata wapi dharau? Ni shetani alitumia Baraka ulizopewa na Mungu kukushawishi hata akakupata na kukupandia roho ya dharau.


iv.                 Hofu ya Mungu hupotea ndani ya mtu.
*1falme11:1-4
habari za mfalme Suleimani ambaye alikuwa na hekima nyingi alizopewa na Mungu. Kupitia hekima hiyohiyo shetani alimshawishi hata mfalme akawa hana hofu tena ya Mungu, akadiriki hata kuoa wake ambao si wa Israel wakati Mungu alikataza, pia kwa kupitia hekima hiyohiyo Seleimani akawa hana hofu tena ya Mungu hata akaanza kuabudu miungu.

MATOKEO YA KUJITENGA NA MUNGU
 Kwa sababu umejitegemea, huna hofu tena ya Mungu, umejaa dharau na Kiburi Mungu hakuachi ulivyo lazima akurudi kwa ,
i. kukulaani
*Ezekiel 26:19
“Bwana Mungu asema hivi nitakufanya kuwa mji wa ukiwa, kama miji isiyokaliwa na watu….”
Mungu hakuiacha Tiro aliipiga hata ikawa ukiwa na ndo maana hata wakati wa Yesu, Yesu aliusikitikia mji wa korazini na Bethsaida kwa kuilinganisha na Tiro mji wenye kiu ya kusikia na kumpokea Yesu lakini Tiro na Sidoni ni Ukiwa( luka 10:13-14). Na ukiwa huu ulitoka toka enzi za nabii Ezekiel kama tulivyoona hapo awali.
ii. kukupiga kwa magonjwa,vita au njaa
* 2samweli 24:15
baada ya Daudi kuhesabu Israel Mungu hakumwacha Daudi akampiga kwa Tauni.
Usije ukashangaa kabla hujawa na mali nyingi magonjwa yalikuwa hayakutembelei, ghafla ulipobarikiwa nyumba yako imegeuka kuwa ghala ya magonjwa.
Na wakati ulipokuwa hujabarikiwa ndoa yako ilikuwa na amani baada ya Baraka ndoa haina amani, watoto haweeleweki n.k

iii. kunyang’anywa cheo
1falme 11:1-
kwa kosa la Seleimani basi ukoo wa Yuda ukanyang’anywa ule uwezo wa kuwa ukoo wa kipee wa kifalme kwa taifa la Israel, ufalme ukagawanyika katika makundi mawili, kundi lenye kabila kumi  na kundi lenye kabila mbili, na ukoo wa Yuda ukaendelea kuwa wa kifalme kwa makabila mawili tu.  Yote hii ni kutokana na makosa ya mfalme Suleimani.

ANGALIZO
Haina maana kuwa usifanikiwe na usitafute Baraka za Mungu la hasha, unatakiwa ufanikiwe tena kwa kiwango cha juu kuliko hata wa mataifa maana wewe uliyeokoka ni mtoto wa mfalme (Mungu), na Mungu ndo mwenye kila kitu duniani hivyo kama mwana wake una haki ya kumiliki mali ya babako. Ila kadiri unavyofanikiwa wewe zidisha hofu ya Mungu ndani yako na uwe mtiifu kwa Mungu hata kufa pia uwe wa kujishusha mbele za Mungu siku zote ila uwe juu ya shetani siku zote.
Mkumbuke Daniel pamoja na matukio mengi mazuri aliyopata na kupitia lakini alibaki kuwa mtiifu kwa Mungu mpaka kufa.

Jizoeze na kuwa na ushirika na Mungu aliyekupa hiyo baraka, yaani mjali Mungu aliyekupa hizo baraka kuliko kuijali hiyo baraka, maana baraka itaisha,koma,pungua, badilika n.k,  lakini aliyekupa baraka haishi, hapungua na wala habadiliki. Moyo wako siku zote umwelekee aliyekupa baraka yaani Mungu, na wala moyo wako usiegemee kwenye baraka.

Mungu akubariki kwa kuachilia muda wako na kusoma somo hili.
ahsante
Doris Barnabas ( Mrs. Daniel Kulwa)

























4 comments: