Wednesday, 30 May 2018

SOMO


OF JESUS CHRIST


NEEMA YA BWANA YESU

UTANGULIZI

Kabla hatuajaenda ndani zaidi hebu fuatana nami kwa kusoma mistari hii;

2koritho 13:14
Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo
wa Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae
nanyi nyote”
Rumi 16:24 & 2Thesolonike 3:18
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe
nanyi nyote”.

Galatia 6:18, filipi 4:23& filemoni 1:25
Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu
Yesu Kristo ikae pamoja na roho zenu.”
Efeso 6:24
Neema iwe na wote wampendao
Bwana wetu Yesu Kristo kwa pendo wa dhati

Karibu kila mstari ambao Paulo alikuwa anawaandikia kanisa wa mahali mbalimabali ulimwenguni alikuwa anahusanisha maneno “Neema ya Yesu Kristo”
Je umewahi kujiulizaau kutafakari ni kwanini
·         Paulo alikuwa anarudia rudia haya maneno karibu nyaraka zake nyingi.
·         Je hii ilikuwa ni sehemu ya maombi ya Paulo akiwaombea watu wa kanisa?
·         Zilikuwa ni Baraka Paulo alikuwa anawabariki watu wake?
·         Kwanini mara zote alikuwa anasema Neema ya Bwana Yesu Kristo na asiseme Neema ya Mungu au Neema ya Roho Mtakatifu?
Katika nyaraka  tulizopitia hapo awali, Paulo alikuwa natafautisha vitu vitatu na nani mhusika kwa kila kimoja. Tazama pale aliposema “Neema” alisema ni ya Yesu kristo, aliposema “Pendo” aliunganisha na Mungu na aliposema juu ya” Ushirika” alimtaja Roho Mtakatifu.


MUNGU NI PENDO

Hapo mwanzo Neno alipokuwa ndani ya Mungu , Mungu alimtoa Neno toka ndani yake, naye Neno akachukua mwili na kuja kwetu akaja kwa jina la Yesu (Yohana 1:1-4,14). Kile kitendo cha Mungu kumtoa Neno aje kwetu kilikuwa ni cha upendo, alitupenda sisi kuliko hata mwanae ( Yohana 3:16) hakuona thamani ya mwanae kuwa ni kitu kwake, bali thamani yangu mimi na wewe ndio aliona ni kitu cha thamani kwake.  Sasa Mungu mwenyewe ni PENDO ndani ya huyu Pendo kumezaliwa karama yake ya Upendo. 

Yesu hakuja kwetu duniani sababu alikuwa anatupenda, bali alikuja duniani kwa sababu ya KUMTII Baba yake (Ebrania 3:2 na Filipi 2:8). Yesu alikuwa na Upendo kwa Baba yake hata akakubali kutii hata kufuka kifo cha msalaba. Kifo cha msalaba hakikupngwa na Yesu bali na Mungu mwenyewe kwani ndiye aliyekuwa na Penzi/Pendo kwa mwanadamu. 

Tazama hata Yesu mwenyewe alipokuwa anazungumza na wanafunzi wake, aliwaambia ” Kama vile Baba alivyonipenda Mimi, hivyo ndivyo Mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo Langu”  kuwa yeye (Yesu) hakuwa na upendo kwetu, ILA sababu na kwakuwa BABA yake alikuwa anampenda yeye ( mwanae) basin a yeye (Yesu) akajikuta/akawahana budi kutupenda sisi. Kwa lugha rahisi ni kuwa Pendo la Yesu Kwetu limesababishwa na Mungu kwanza kumpenda Yesu. Ila Pendo la Mungu kwetu halina sababu.

Hivyo Paulo anaposema juu ya Pendo anamaanaisha ni Mungu tu ndiye awezaye kukupenda mwanadamu bila sababu au kuchochewa na chochote.  Na ni yeye peke yake mwenye hiyo hali ya Kupenda.

ROHO MTAKATIFU NI MSHIRIKA.

Biblia katika mistari tuliyosoma hapo awali, inasema juu ya ushirika kuwa u ndani ya Roho Mtakatifu.
Yohana 14:26
Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye
Baba atamtuma kwenu kwa Jina Langu,
atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha
yote niliyowaambia.

“Huyo Msaidizi” maana yake ni wa karibu, mwandani, kipenzi, mshirika au mbia. Kama ni mwandani wako ina maana mnashirikiana katika kufanya “kitu/jambo”.
Rumi 8:9
Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na
Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani
yenu. Mtu ye yote ambaye hana Roho wa
Kristo, yeye si wa Kristo.
Rumi 8:14
Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu hao ndio
watoto wa Mungu.

Kama Roho Mtakatifu anakaa ndani yako na pia unaongozwa naye katika kila jambo, ile tu kuongozwa naye na wewe kukubali kukuongozwa ina maana kuna tendo la ushirika kati yenu.Nachelea kuendelea mbele zaidi juu ya Roho Mtakatifu maana ni somo pana litakuja kwa wakti wake. Ila uelewe kuwa mwenye USHIRIKA na mwanadamu ni Roho mtakatifu.
Kwa hiyo kama Pendo ni Mungu, Ushirika ni Roho Mtakatifu basi Neema iko kwa Yesu Kristo kama Paulo alivyowaandikia makanisa mbalimbali. Naomba nikukumbushe kuwa somo letu ni juu ya Neema ya Yesu Kristo.

NINI MAANA YA NENO NEEMA

Neno neema ni pana sana na linaweza kuchukuliwa tafsiri kwa kulingana na tukio. Hizi ni baadhi tu ya maana ambazo tutaenda nazo katika hili somo.


  • ·         Ni kusaidiwa,kupewa msaada pale usipoweza au uliposhindwa ( helpful)

  • ·         Ni kujali,kupewa uangalizi wa pekee,  ( to care)

  • ·         Kustahilishwa yaani unapewa stahili ambayo kihalali hukustahili/ hukutakiwa kupewa.

  • ·         Kupendelewa, kupewa upendeleo katika jambo Fulani ambalo kwa utaratibu na uhalali hukustahili wewe kupata hilo jambao.

Yesu ndie ataoae neema kwa wanadamu. Tazama maana ya “neema” kupitia mifano hii;
  1.         i.            Mungu pamoja na pendo lake huwa hachangamani na wenye dhambi (Yohana 9:31). Na kama hawezi (Mungu) kuchukuliana na mwenyedhambi nani wa kusimama kati ya mwanadamu mwenye dhambi na yeye? Maana mshahara wa dhambi ni mauti, ile tu kwamba umetenda dhambi basi, unastahili mauti ya vyote roho na mwili. Ndipo Yesu hutustahilisha mbele za Mungu kwa damu yake, anachosema mbele za Mungu kwa niaba yako ni kuwa “ ndio huyu Fulani kafanya dhambi hii na hii nah ii na anastahili kufa, LAKINI kumbuka nilikununulia na huyu Fulani kwa Damu yangu (Ufunuo 5:9), hivyo anastahili kupewa muda wa kutengeneza, usimue ( Luka 13:6-9). Hivyo pamoja na dhambi hufi ila umepewa upendeleo wa kuendelea kuishi wakati kiutaratibu wa Biblia usingepaswa kuendelea kuishi. Hii ndio Neema ya Yesu Kristo.

  1.       ii.            Wewe ambaye ni taifa nje ya Israel ( kimwili) haukupaswa kumkaribia Mungu, maana ulikuwa umelaaniwa kabisa, hukustahili hata kuliitia jina la Mungu wa Israel. Ndio maana biblia inakuita wa mataifa, yaani nje ya Israel. LAKINI baada ya kufa na kukufuka kwa Yesu Kristo akatuondolea laana tulioitwa wa mataifa akatuingiza katika zizi la Ibrahimu (Galatia 3:13-14, 29), kisha akatuistahilisha mbele za Mungu hata leo tunathubutu kuliitia jina la Mungu wa Israel, ooooooh haleluyaaaaa!! Sifa kwa Mwanakondoo aliyetununua kwa Damu yake.

  1.     iii.            Anapendelewa hata mbele ya mahakama ya mbinguni maana kwenye kitabu cha

Ufunuo 12:10-11
“Kisha nikasikia sauti kuu mbingunii kisema,Sasa Wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja na mamlaka yaKristo wake. Kwa kuwa ametupwa chini mshtaki wa ndugu zetu,anayewashtaki mbele za Mungu usiku na mchana.
11 -Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo na kwa neno la ushuhuda wao. Wala wao hawakuyapenda ……”

Kwamba, katika maisha ya mwanadamu ya kila siku ukikosea, shetani anawahi mbinguni kwenye mahakama anapeleka mashtaka kuwa Fulani amefanya hivi na vile, anastahili mimi (shetani) nimmiliki na nimfanyie ninavyotaka. Mashatka haya yanapopelekwa wewe huku duniani hujui na unaendelea na shughuli zako. Ndipo Yesu anatumia Damu yake mbele ya mahakama kuwa, ndio alitenda hiki na hiki LAKINI, Damu yangu ( Yesu) imelipa hayo yote na nimemnunua kwa hiyo Damu hivyo Mungu itazame Damu yangu ( Yesu) badala ya hayo mshataka ya shetani. Na Mungu naye anataza kifungu anakutana na Ebrania 12:24 inayosema “Damu ya Yesu inanena Mema” Mungu hasiti kuifutilia mbali kesi kuwa shetani sioni mashataka ya msingi juu ya huyu Fulani, mimi (Mungu) naona Damu inayonena mema juu yake. Unajikuta unashinda kesi wakati wewe huna habari kuwa kuna mahakama inaendelea juu yako. Yote hiyo ni Neema ya Yesu Kristo.
  1.     iv.            Bila Jina Yesu usingestahili kuwa na Roho Mtakatifu ndani yako, na Roho Mtakatifu haji kwako tu sababu wewe umefanya kitu Fulani kizuri, bali Roho Mtakatifu huja mahali palipo na Jina la Yesu .
Yohana 14:26
“Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina Langu,atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia”
Kwamba, yeye Yesu baada ya kufa ni yeye aliyekuchagua wewe na akakupa Jina lake. Ile tu kukupa jina lake, Roho Mtakatifu anakuja penye jina la Yesu. Mungu hamtumi Roho Mtakatifu kwakao sababu umeokoka muda mrefu au sababu unatoa sadaka sana au sababu unapenda kuomba. Mungu anatazama palipo na Jina la Yesu. Hivi ni baadhi tu ya mfano wa namna ambavyo Yesu amejaa Neema kwako.
  1.       v.            Hii Neema ya Yesu inaenda mpaka kwenye maisha ya kila siku, kula kwako, kulala, kuamka, kuembea ni Neema ya Yesu. Hauna uwezo wowote juu ya hayo mambo ila ni Yesu tu ndio anakuwezesha.
Neema ya Yesu Kristo ndio inayokuunganisha na Pendo la Mungu, ushirika wako na Roho Mtakatifu hata kukupa mahaitaji yako yote. Unaishi sababu ya Neema yeke.

TUNAPATAJE NEEMA YA YESU KRISTO?

Kupitia hiyo mifano tumeona namna ambavyo maisha yetu hayawezekani kuendelea mbele pasipo Neema ya Yesu Kristo. Swali je Neema ya Yesu kristo inapatikana kwa kuiomba, kuifanyia tendo lipi hasa.
Ili mradi imeitwa Neema, ina maana unapewa wakati hujakidhi matakwa na viwango vya kupata hicho kitu. Neema hutolewa kwa matakwa (discretions) ya mtoaji. Huwezi wewe mpokeaji kwenda kulazimisha au kuomba kuwa nipe jambo Fulani, na kama umepewa baada ya kuomba hiyo si neema bali ni haki yako.
Haki ni kile kitu ambacho unapata sababu tu aidha umekidhi masharti Fulani au kwa hadhi yako basi unastahili kupata hiyo haki. Unapoomba kitu lazima uwe umejua kuwa umekidhi matakwa au kwa hadhi yako unastahili kupata. Neema ni kinyume cha haki, kwakuwa hujakidhi matakwa na pia hadhi yako haikuruhusu kupata lakini unapata.
Hebu tutazame mfano huu
  1. 1)      wa Zaburi 23:1 inasema Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu. Sasa mtu ambaye amekidhi viwango wa kuwa kondoo wa Bwana, huyu akipewa chochote au asipopungukiwa atakuwa amepewa haki yake, sababu amekidhi matakwa ya Kondoo. Yule ambaye hajakidhi matakwa yaani maisha yake ni ya ki mbuzi mbuzi na sio kondoo, pale ambapo atapewa kitu au hatapungukiwa kitu, huyu sio haki yake na hata alipoomba hakupewa sababu ya kuwa na haki, bali Huruma ( Neema) ya mtoaji ndio imempa hicho.

  1. 2)      Wa mfungwa ambaye kafungwa gerezani kwa miaka kadhaa, ijapo sheria za nchi zinamruhusu raisi kuwatangazia msamaha wafungwa ambao wamekidhi viwango na masharti Fulani. Lakini ni matakwa ( discretion) ya raisi kumsamehe mfungwa Fulani na kumwacha mwingine ambaye makosa na miaka inafanana ya Yule aliyesamehewa. Huyu ambaye hajasamehewa hawezi kulalamika na kudai mahakamani kuwa na yeye afunguliwe. Pamoja na huyu aliyefunguliwa kupewa msamaha, hawezi kusema kuwa ilikuwa ni haki yake kuachwa huru eti   kwa sababu amekidhi matakwa, swali litakuja na yule aliyeachwa ndani na wakati amekidhi matakwa?

Sasa hebu tuangalie biblia inasemaje juu ya kupata Neema ya Yesu Kristo.
Ebrania 4:14,16
14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana
wa Mungu, basi na tuyashike sana maungamo yetu.
16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

Turejee mfano 2 hapo juu huyu mfungwa anapoingia gerezani siku ya kwanza, anaanza kutumikia kifungo chake akijua kuwa uhuru wake utapatikana muda wa kifungo ukiisha. Akiwa katika mchakato wa kutumikia kifungo anaanza kutii mafunzo na masharti yote ya bwana jela, anatii hayo si kwa sababu anataka kupewa uhuru mapema, bali ni kwa sababu ya masharti ya kifungo chake. Akilini mwake anaendelea na maisha ya ufungwa bila kutegemea kuwa kuna siku ataachiwa huru kabla ya muda kufika. Mtoa uhuru wa huyu mfungwa anatazama maisha ya mfungwa ya kila siku, haya maisha ya kila siku ndio humshawishi mtoa uhuru kuachia neema ya uhuru.
Sasa kutoka katika Ebrania 4, tuliyoisoma inaonyesha kuwa kuna maisha Fulani ya mwanadamu ukiyaishi, na katika mchakato wa kuishi hiyo namna ya maisha, basi Neema ya Kristo inakufikia pasipo yeye kuitarajia. Waebrania anataja mfumo wa maisha ya namna hii-;

  1.       KUSHIKA SANA MAUNGAMO.
Maungamo ni ukiri, yaani maneno yatokayo katika kilindi cha moyo wako ambayo yamebeba uhalisia wa moyo wako. Maana hakuna neno ambalo mwanadamu akatamka kama halijatoka katika kilindi cha moyo wake. Biblia inasema kimjaacho mtu ndicho kimtokacho (Luka 6:45) na aonavyo mtu ndani ya nafsi yake ndivo alivyo (Mith23:7). Kwa kila neno unalolisema ujue ndivyo kulivyo ndani ya moyo na nafsi yako.

Ebrania anasema tuyashike maungamo yetu, kuwa kusema kwa nje kunatokana na ndani kuko vipi, na unatakiwa kuchunga sana ndani yako kuna nini. Kilichondani yako ndicho unachokikiri na kinatokea kama unavyokikiri. Haijalishi mdomo utakuwa umeufunga au unatoa maneno, bali ukiri utabaki palepale nafsi yako inaonaje hilo jambo.

Kwa kuwa ndani ya mtu(nafsi) ndiko ukiri hutokea, basi inategemea hiyo nafsi imejaza nini. Kama imejaza unyonge na kushindwa ujue ukiri wake utakuwa hivyo. Na kama nafsi imejaza ushindi na Neno la kristo ujue ukiri utakuwa wa ushindi. Si unajua akuwa chanzo cha imani ni kusikia, chanzo cha imani katika Kristo ni kusikaia Neno la Kristo (Rumi 10:17). Nafsi inajazwa na kile ilichosikia, na ikishajaa ilichosikia ndipo hapo nafsi huanza kutema/kukiri yaliyojaa ndani yake. Ukitaka kujua moyo wa mtu umejaa nini sikiliza maneno yake, kama umejaa mpira wa miguu muda wote hana mazangumzo mengine ni hayo tu, umejaa ushirikina muda wote atakuwa anazungumza juu ya uchawi na waganga.

Kama amejaza Neno la Mungu hata kama hajasema mstari wa biblia ila maneno yake yatakuwa ni ya hekima na Yesu huwa na huyo mtu muda wote, maana Yesu ndio Neno lenyewe na pia Injili ya Yohana inasema maneno yangu ( Yesu) yakikaa ndani yenu, Yeye Yesu na Baba watakaa ndani ya huyo mtu . Kama Yesu, Baba na Roho Mtakatifu wanakaa ndani ya huyo mtu ujue huyo mtu atakuwa anastahilishwa na kupendelewa katika maisha yake.

Imani chanzo chake ni kusikia Neno la Kristo. Na imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo ni bayana ya yale yasiyoonekana (Ebrania 11:1) maana yake  ukilipokea Neno ndani yako linakupa uhakika wa hilo jambo sawa na Mungu aonavyo juu ya hilo jambo, hivyo ukiri wako unakuwa sawa na Neno na unakuwa ni ukiri wenye kuumba vitu vyema na  vikatokea. Maana kwamba Neema ya Kristo inakuwa imetolewa (Neno), ukilipokea Neno Yesu anakusaidia namna ya kulifanya hilo Neno liwe hai, ile Yesu kukusaidia kulifanya Neno kuwa hai ndio Neema.

Kwa lugha rahisi ni kuwa Yesu anaachilia Neema, Imani yako ndio mrija wa kupokea na kupitisha Neema. Mfano kifo cha Yesu msalabani hii ni neema kwa Mataifa, na hii Neema ilikwisha kutolewa kwa kila mtu, sasa mwenye Imani akilipokea Neno la msalaba ndani yake, Yesu anamsaidia kulifanya hilo Neno kuwa hai, ndipo tunamwita huyo mtu ameokoka.
Ebrania anatutaka tuwe makini na ukiri wetu kwa maana huo ukiri ndio unaokusaidia kupata neema wakati wa uhitaji. Yaani usipate shida wewe jaza Neno la Kristo ndani yako liishi hilo Neno, ujue nyakati za uhitaji ukiri wako wa kila siku utakufanya upate upendeleo na msaada       ( neema) toka kwa Yesu. Utakuwa sawa na mfano wa huyo mfungwa ambaye anaendelea kuishi kama bwana jela atakavyo bila kujua na kujali kuwa kuna siku atatangaziwa uhuru kabla ya muda. Usijaribu kuigiza katika ukiri wako, maana kikujazacho ndicho kikutakacho, na ukijaribu kuigiza ukiri ili baadae uombe utakuwa sawa na yule farisayo alikuwa anaomba kuwa yeye anafunga mara kadha kwa wiki na pia sio kama Yule mtoza ushuru (Luka 18:9-14) sahau kupokea majibu ya maombi yako.
Kumbuka mwenye haki anaishi kwa imani yake ( Ebrania 10:38) neema itakukuta njiani wakati unapoendelea kuishi kwa Imani, na Neema inakuja kukusaidia pale usipostahili au usipoweza.


2.      KUKARIBIA KITI CHA REHEMA

Kiti cha Rehema ni nini
Kutoka 25:17-22
17 nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi, chenye urefu wa dhiraa mbili na nusu naupana wa dhiraa moja na nusu.
22 nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha Rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israel.

Mungu alimwelekeza Musa namna ya kujenga hema ya kukutania, katika vitu ambavyo alimwelekeza weke ndani ya Patakaifu sana, kimoja wako ni kiti cha Rehema. Hiki kiti kiliwekwa juu  sanduku la agano, mstari wa 22 unaeleza kusudi la kuwepo kwa kiti cha Rehema kuwa itakuwa ndio sehemu ambayo Mungu ataonana na kuzungumza Musa mahali pale. Ina maana Musa alipotaka kuzungumza na Mungu hakuenda tena mlimani kama hapo awali bali aliingia patakatifu na kukaribi kiti cha Rehema.

Hayo yalikuwa wakati wa agano la kale.Yesu alipokuja siku ya kufa kwake, pazia la hekalu lilipasuka vipande viwili (Math 27:51) kumaanisha kuwa patakatifu sana pa dunia hapatakuwa tena katika hekalu lililojengwa kwa matofali, nondo n.k. maana Sanduku la agano lilitolewa duniani liko mbinguni (Ufunuo 11:19). Kila mtu aliyempokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wake amepewa ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa kupitia Damu ya Yesu ( Ebrania 10:19-20).

Kiti cha rehema hata sasa kipo na halisi huko mbinguni, soma

Ufunuo 8:3 inasema
3 Malaika mwingine aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, akaja na kusimama mbele ya madhabahu.Akapewa uvumba mwingi ili autie pamoja na maombi ya Watakatifu wote, juu ya
ile madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele ya kile kiti cha enzi.

Kumbuka kazi ya Kiti cha Rehema cha kipindi cha Musa ilikuwa ni Mungu apate kuona na kuzungumza na Musa hapo. Na tafsiri rahisi ya maombi ni mazungumzo kati ya Mungu na mwanadamu. Ufunuo anasema huyu malaika anayachukua maombi ya watakatifu kisha anayachanganya na uvumba anafukisha juu ya kiti cha enzi.Maombi ya watakatifu huwa yanapokelewa katika eneo liitwalo kiti cha Enzi. Mazungumzo ya Musa na Mungu ni kwenye kiti cha rehema, na mazungumzo ya watakaifu na Mungu ni kwenye kiti cha Enzi.
Kiti cha rehema kilikuwa kwenye madhabahu ya uvumba, na kiti cha Enzi kiko kwenye madhabahu ambayo pia kuna uvumba.
Hivyo kiti cha rehema kipindi cha agano la kale kilikuwa ni kivuli cha kiti cha enzi mbinguni.

Tukirudi kwenye Ebrania 4:16 anasema “…tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia..”
 Ina maana Maombi, mazungumzo kati ya mwanadamu na Mungu, ndio njia inayomfanya mwanadamu kukisogelea kiti cha enzi na hicho kiti kimejaa neema ambayo huachilia rehema na hupelekea huyu mwanadamu kupata neema ya kusaidiwa wakati wa uhitaji.

Haina maana kuwa ukiendee kiti kwa ajili ya kuomba neema, ina maana unapokiendea kiti kwa ajili ya haki yako au jambo lako lolote. Unapoendelea kuzungumza na Mungu juu ya hilo jambo, Yesu anaachailia neema itakayokusaidia wakati wa uhitaji, hivyo wewe uliendea kiti kwa jambo lingine ukitoka kwenye kiti unarudi na neema ya kusaidiwa nyakati za uhitaji.
Kwa kadiri unavyokiendea kiti kwa ajili ya mazungumzo na Mungu ndivyo unavyozidi kuongeza neema ya kukusaidia wakati wa uhitaji.

Tazama Yesu alipowaambia wanafunzi wake,kesheni mwombe msije mkaingia majaribuni (Mathayo 26:41). Hakumaanisha wakeshe na waombe wasiingie majaribuni, alikuwa anawahimiza kuwa endeleeni kuzungumza na Mungu juu ya maisha yenu na mtakapokuwa mnaendelea kuzungumza na Mungu, mtapokea neema ambayo hata jaribu kilikija halitakuwa jaribu kwenu maana mna msaada wa ziada wa kuwafanya lisiwe jaribu kwenu

HITIMISHO
Usijaribu kuomba Yesu akupe neema, Neema haiombwi anatolewa jinsi apendavyo yeye  (Yesu). Wewe unapaswaa ubadili mfumo wa maisha yako, uishi maisha ya Imani, yaani kulitii Neno na kuwa halisi kama Neno liatakavyo. Ukiweka nia na kiu ya kuliishi Neno yeye Yesu ataachilia Neema yake ya kulipata, kulielewa na kuliishi Neno. Kwa maana huwezi kuliishi Neno kwa akili na nguvu zako.

Pia Maombi kwa uongozi wa Roho Mtakatifu yawe ndio maisha yako ya kila siku, muda wowote na popote pale ulipo.

USHAURI
Kwa wewe ambae unasoma somo hili na hujampa Yesu maisha yako awe Bwana na mwokozi wako, kumbuka Neema yake imekwisha kutolewa ni wewe tu Kuamini na kukubali na kumruhusu Yesu aingie ndani yako. Usiogope utaishi vipi maisha ya wokovu. Wewe amini kuwa alikuja duniani na akafa kwa ajili yako,na kiri kwa kinywa chako kuwa umwenye dhambi na unaomba toba ( geuka) na mruhusu atawale maisha yako. Yesu atachilia Neema itakayokusaidia kukua katika wokovu.

Kama uko tayari omba sala hii
“ Yesu mimi ni mwenye dhambi, nisamehe dhambi zangu. Nilikuwa mbali nawe narudi kwako, nipokee kama mwana wako.nakubali kukupa moyo, nafsi na mwili wangu viwe vyako kwa ajili yako. Amen

Kama umefanya sala hii kwa kumaanisha, tayari umeokaka na Yesu yu pamoja nawe akusaidi.
Hongera kwa kuokoka.

Ni Mimi mwalimu wa injili
Mrs. Doris Barnabas Daniel

No comments:

Post a Comment