MALEZI & VIJANA



MTOTO WAKO YUKO HIVYO SABABU WEWE UMEHUSIKA AWE HIVYO





 

UTANGULIZI

Umewahi kujiuliza maswali haya;

i.                    Kwanini wewe ni mama au baba wa huyo mtoto?


ii.                  Kwani nini hao watoto walizaliwa kwenye tumbo lako au kwenye viuno vyako?


iii.                Au kwanini hao watoto wasizaliwe kwenye tumbo la mwanamke mwingine au viuno vya mwanaume mwingine


iv.                Au kwanini watoto wa jirani yako hawakuzaliwa kwako? Na wako wako wasiwe wa jirani yako


v.                  Uliwahi kuchagua mtoto huyo apite kwako na mwingine apite kwa jirani yako?


Wengi wanadhani kuwa, kwa kuwa ni basi wazazi wana wajibu wa kuhakikisha wamewapa na kuwatimizia watoto wao mahitaji yote ya mwili na elimu mpaka watakapokuwa watu wazima na wenye uwezo wa kujitegemea. Wengine huendelea mbele zaidi kwa kuwaandalia mali za kurithi ikiwa ni kuwafungulia biashara na kuwapa mitaji, nyumba nzuri na vingine vifananavyo vya hivyo. Ni sawa kabisa na hatuko kinyume na neno la Mungu maana


v  Mithali 19:14 inasema;


Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana”


Je hata katika hili wazazi tumekuwa waaminifu kulifanya kwa watoto wetu. Kwa mstari huu ina maana mzazi mwenye watoto watatu unatakiwa uwe na nyumba zisizopungua nne, tatu zikiwa za watoto wako na moja yenu wazazi, waweza kuzidisha nyumba lakini chamsingi zisiwe chini ya nyumba nne. Kadhalikia kwa wazazi wenye watoto watano wasiwe na nyumba chini ya sita. Ina maana mtoto atakapo kuwa mkubwa umkabidhi nyumba yake na mali ya kuanzia maisha. Mzazi una jukumu la kutafuta mali kwa ajili ya mtoto wako


Kama mtoto anatakiwa arithi ardhi nyumba na mali toka kwa baba yake,  je wajibu wa Mzazi kwa mtoto ni kumtafutia mali tu, Na kuhakikisha awapo mkubwa mali ziwe tayari zinamgojea? La hasha! Biblia imempa mzazi majukumu mengi ambayo anapaswa kuwajibika kwa ajili ya mtoto wake. Kuwa mzazi ni sawa na Mungu kukwambia kuwa unatakiwa ujue na ufanye haya yafuatayo:


1.      KUSUDI LA MUNGU KUMUUMBA HUYO MTOTO


AU MTOTO WAKO NI NANI

Ili mzazi asimame kwa zamu yake mbele za Mungu anatakiwa kujua kuwa mtoto aliyenae ni nani mbele za Mungu sina maana kujua kuwa ni wakiume au wakike, hilo halina shida kabisa maana Mungu hatazami jinsia ya mtoto anatazama roho ya mtoto. Mungu ni Roho nao wamwabuduo imewapasa wamwabudu katika roho, hivyo Mungu hushughulika na roho ya mtu.  Kwa habari ya jinsia, baada ya kufa kwa Yesu watu wote tukaitwa ma bibi-harusi wa Yesu, hapo awali kabla ya Yesu kulikuwa na mwanaume na mwanamke mbele za Mungu, ndo maana hata Wa Israel walipokuwa wakihesabu watu walikuwa wanahesabu wanaume tu. Haleluya kwa ajili ya Yesu ambaye yeye anawaita wote ma bibi harusi wake.


Mzazi unatakiwa kujua kwanini Mungu alimuumba huyo mtoto, haitoshi kuwa na sababu ya kuwa alimuumba ili kuujaza ulimwengu ( mwanzo1:28) . Mungu amemuumba kila mtoto kwa kusudi lake, na hakuna kusudi la mtoto linalofanana na la mtoto mwengine. Mungu hajawahi kutoa nakala (photocopy) ya mtoto yoyote, hata kama kimaumbile ya mwili watoto ni mapacha au sio mapacha ila wanafanana sana bado hawatakuwa na kusudi mmoja la kuja hapa duniani. Ukilijua kusudi la mtoto wako kuletwa na Mungu duniani, utajua namna ya kumwombea, kumlea katika njia ipi au hata namna ya kumlisha chakula.


Ni wajibu wako mzazi kumjua mtoto wako ni nani (yaani kusudi la Mungu kumuumba huyo mtoto) akiwa bado yuko tumbo hata kabla hajazaliwa. Kumbuka Rebeka mke wa Isaka alipokuwa mjamzito alimuuliza Mungu juu ya uja uzito wake maana aliona mapambano yanayofanyika ndani ya tumbo lake ni makubwa mno. Ndipo Mungu alimwambia mapema kuwa ni mataifa mawili na Yule mkubwa atamtumikia mdogo (mwanzo 25:21-23). Mzee Isaka alipotaka kumbariki Esau aliye mkubwa sawa na desturi za watu wote, Rebeka akaingilia kati akamfundisha Yakobo “ aziibe” Baraka za Esau (mwanzo 27:1-33). Ni rahisi sana kumchukia Rebeka kuwa alimfundisha mwanae aibe Baraka za kakake, lakini si hivyo Rebeka alijua siri ya wanae wawili kuwa lazima mkubwa amtumikie mdogo na hiyo siri hakumwambia mumewe maana kama alikuwa amemwambia Isaka asingetaka kumbariki Esau. Rebeka hakutaka Isaka afanye tofauti na neno la Mungu, ni Mungu mwenyewe ndiye aliyemchagua Yakobo kuwa awe mkuu na Esau amtumikie. Kwa kulijua kusudi hili Rebeka akawajibika sawasawa ili Yakobo awe mkuu na Esau awe mtumwa wake. Usimchukie Rebeka kwani alikuwa kazini kuhakikisha kusudi la Mungu linatimia kwa wanae wote.


Pata picha wewe ni mzazi wa Samsoni, kila kukipambazuka unapokea mashtaka toka kwa majirani zako kuwa Samsoni kachoma moto mashamba ya watu, mara Samsoni kauwa watu, mara kawanyang’anya watu nguo zao. Kubwa kuliko zote anakujia Samsoni mwenyewe na kukwambia kuwa anataka kuoa binti wa kifilisti. Na wakati huo Mungu amekuagiza kuwa usimpe mtoto wako wa kiume mke nje ya kabila la Israel na usimwozeshe binti yako kwa kabila nje ya Israeli. Na kila ukimwelewesha Samsoni juu ya hilo agizo la Mungu yeye hakuelewi ameng’ang’ania tu amuoe huyo binti. (waamuzi sura 13,14,15&15). Ni rahisi sana kwako kuanza kukemea na kufunga ili hiyo roho imtoke, na kila ukiomba unashangaa roho haimtoki ndio kwanza anazidi kufanya mabaya zaidi kwa majirani zako. Mzee Manoa na mkewe haikuwasumbua tabia ya Samsoni wala hawakusumbuka kumkataza maana walijua kusudi la Samsoni kuzaliwa  ili alikomboe taifa la Israeli toka kwa wafilisti (waamuzi 13:4-5,12-14). Yakimkini walipoletewa mashtaka wao waliingia ndani nakumshukuru Mungu kuwa safi sana Samsoni kawakomesha wafilisti. Waliweza kushukuru kwa Mungu sababu walijua kazi moja ya Samsoni ni kuwakomboa Israeli toka kwa wafilisti, hivyo ushindi wowote alioupata Samsoni toka kwa Wafilisti wao walishangilia na kumshukuru Mungu.


Wengi wetu tuna akina Samsoni katika maisha yetu, tunashughulika kufunga na kukemea roho zilizondani yao kwa kuwa tu hazikupendezi mzazi lakina hatujui kuwa Mungu yuko kazini ndani ya mtoto wako, anamtumia Samsoni wako ili alete ufalme wake duniani. Sina maana kila mwenendo mbaya wa mwanao basi ni kusudi la Mungu, lahasha! Nataka nikwambie kuwa ukimjua mwanao ni nani haitakusumbua anachofanya ili mradi kiko katika kusudi la Mungu. Wazazi wengi hawawajui watoto wao hivyo hawajiu kama mwenendo wao uko katika kusudi la Mungu au hapana.




Mpendwa Mungu haumbi mtoto kwa bahati mbaya wala kwa kubahatisha. Haijalishi mimba ya mtoto ilitungwa hali ya dhambi, bado Mungu anamakusudi na huyo mtoto. Dhambi za baba na mama hazimfanyi mtoto awe najisi mbele za Mungu.


v  Zaburi 51:5


Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani.”


Huyu ni Daudi anayesema mimba yake ilitungwa hali ya dhambi, lakini Mungu alimpenda Daudi na alimkusudia awe mfalme wa Israeli. Kusudi la Mungu kwa mtoto analiweka ndani ya mtoto hata kabla mtoto hajazaliwa wala mimba yake kutungwa. Najua unajiuliza nimejuaje, nimejua kwa kuwa kitabu cha

v  Yeremia 1:5

“Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.”


Kujua ni ile hali ya kuelewa jambo Fulani au mtu Fulani na kuwa na mahusiano wa (kimatendo) naye ya kibinafsi na huyo mtu. Sasa Mungu anamwambia Yeremia kabla sijakuumba nalikujua, ana maana kabla hajamuumba Yeremia Mungu alikuwa ana uhusiano binafsi na Yeremia. Najua unashangaa, iweje Mungu awe na uhusiano binafsi wa kimatendo na Yeremia wakati bado hajaumbwa. Ni sawa Mpendwa kabla Mungu hajamuumba mwanadamu Mungu anakuwa na mahusiano naye kumbuka Mungu ni Roho na wote wamwambuduao imewapasa wamwabudu katika roho, sasa kabla hajamuumba mwanadamu Mungu anakuwa na uhusiano naye katika ulimwengu wa roho. Mungu ana uhusiano na roho na sio mwili, kabla hujaupata huo mwili Mungu anakuwa amekwisha kuwa nawe. Mungu alikuwa na uhusiano na Yeremia hata kabla yeremia hajakuwa katika ulimwengu wa mwili. Mungu alipandana na kuweka roho ya unabii ndani ya Yeremia hata kabla Yeremia hajawa mwanadamu katika mwili.

Wazazi wengi wanadhani kazi au huduma za watoto wao zinawekwa ndani ya watoto wao kipindi cha kuzaliwa duniani toka tumboni mwa mama zao, au kipindi wawapo wakubwa na wakiokoka. Kazi au huduma  ya mwanao inaumbwa ndani ya mwanao kabla ya mimba yake kutungwa.

v  Luka 1:15,24


15 “ Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho.

24 Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema,”


Huyu ni Yohana mbatizaji, ambaye atakuwa mkuu mbele za Bwana (Yesu), na atajazwa Roho Mtakatifu, malaika alikuwa namwelezea Yohana mbatizaji atakavyokuwa katika ulimwengu wa mwili ina maana katika ulimwengu wa Roho alikuwa ameshakamilika, na wakati malaika akinena hayo Elizabethi hakuwa mjamzito, ndio maana mstari wa 24 unaanza kwa kusema hata baada ya siku zile, ina maana siku zile ambazo malaika alileta ujumbe wa Mungu kupita ndipo Elizabethi akapata mimba ya Yohana Mbatizaji. Kazi na huduma ya Yohana mbatizaji ilikuwa imeshawekwa ndani ya Yohana hata kabla ya mimba yake kutungwa.

Ukijua mtoto wako ni nani utaweza kumwombea sawa na kusudi la Mungu, pia hata kumlea katika njia impasayo. Jihadhari ewe mzazi usiwe kama mzee Yese, Yule baba yake na Daudi. Hakujua kama ndani ya Familia yake kuna mfalme, hata alipoulizwa na Samweli kuwa watoto wako wapo hapa, alijibu amesalia mdogo tazama anachunga kondoo (1Samweli 16:11) Yese alimwona Daudi kuwa ni mdogo na kazi yake ni kuchunga kondoo tu hana kazi ingine. Laiti kama Yese angemjua Daudi kuwa ni mfalme pengine asingemwacha muda wote ashinde maporini kuchunga kondoo.

Usivunjike moyo ikiwa mpaka sasa mwanao amekuwa na umri wa miaka kadhaa bado hujui yeye ni nani. Omba toba kwa Mungu kwa kutosimama katika zamu yako kama mzazi atakiwae kusimamaia kusudi la Mungu ndani ya mtoto wako. Kisha msihi Mungu akufungue upate kujua hayo na akupe hekima namna ya kusimamia na kutunza kusudi la Mungu ndani ya mwanao. Jifunze kuwa msiri juu hayo Mungu atakayokwambia, kama Rebeka alivyoweza kuwa msiri lakini akiwa na bidii kusimamia kusudi la Mungu.Utasamimia kusudi la Mungu ndani ya mwanao kwa kumwombea na kumfundisha njia za kuliendea hilo kusudi (Zaburi 78:5-6). Hata kumfundisha kuchanga aina za ulaji wake wa chakula, kama mzee Manoa alivyofanya. Si kwamba kuna dhambi kwenye ulaji wa baadhi ya vyakula bali kama mtoto wako ni Kiongozi wan chi kwa ngazi yoyote lazima achunge wapi anakula kwa manufaa ya usalama wake, angalia Daniel na waenzie walichunga sana namna ya ulaji wao sababu tu walikuwa wanaandaliwa kuwa viongozi (Daniel 1;8-16). Pia utamfundisha namna hata ya utunzaji mwili wake sawa ni yeye ni ni nani duniani, maana aweza akawa ni kuhani kama Samweli, na huku hatakiwi kunyoa nywele (1samweli 1:11). Mjue mwanao ni nani, msihi Roho Mtakatifu akuwezeshe kumlea sawa na Mungu anavyotaka awe.

      2. SHETANI ANAWEZA KUPINGA KUSUDI LA MUNGU NDANI YA MWANAO:

Kazi kubwa ya shetani ni kuhakikisha kusudi la Mungu halitimii ndani ya maisha ya mwanao. Hii haina maana kuwa Mungu hana kusudi na mwanao. Kusudi la Mungu ndani ya mwanao ni sawa na moto wa kuni, unavyozidi kuuchochea ndivyo unavyozidi kuwaka, ukiacha kuchochea utazimika. Ni wajibu wako mzazi kuhakikisha kusudi la Mungu ndani ya mwanao linatokeza katika ulimwengu wa mwili na linamzalia Mungu matunda mema na aliyoyakusudia Mungu yazaliwe toka kwa mwanao.

Shetani haanzi kupinga kusudi siku ya kuzaliwa kwa mtoto, huanzia toka hata kizazi cha pili nyuma ya kizazi cha huyo mtoto. Hebu taungalie mfano wa kitabu cha Ruthu. Watoto wote wa kiume wa Naomi walikufa kabla hawajazaa watoto. Ruthu ambaye alikuwa mkamwana wa Naomi akaenda kulala na ndugu wa mumewe ili amzalie mumuwe (marehemu) mtoto,maana sheria ya Musa iliwaruhusu kufanya hivyo. Ruthu akamzaa Obedi. Obedi ni baba wa Yese, Yese akamzaa Daudi na Daudi ndio uzao wa Yesu (Mariamu mamaye Yesu na hata Yusufu baba mlezi wa Yesu) Ruthu ni Yule yule ambaye alishindwa kubeba mimba toka kwa mumuwe, na anabebeba mimba kupitia mwanaume mwingine. Shetani alikuwa anawinda kuzaliwa kwa Daudi. Alijua kwa kuwamaliza watoto wa kiume wa Naomi mwisho wake Yese asingezaliwa kadhalika na Daudi. Laiti kama Naomi angelijua kuwa tumbo lake lilibeba hatma ya kuzaliwa kwa Daudi, angeliomba juu ya ndoa za wanae na hali ya uzazi wao.

Kama mzazi umewahi kujiuliza ni muda gani muafaka wa kuombea ndoa ya mwanao? Au je kama mzazi una wajibu wa kuiombea ndoa ya mwanao? Usifikiri kuwa suala la ndoa ya mwanao linamhusu yeye mwenyewe, au muda wa kumwombea aolewe au aoe ni mpaka umri ukishafika wa kuoa au kuolewa, wengine husubiri mpaka umri upite sana ndipo aanza kuomba binti yake aolewe au kijana wake aoe. Na wengine hudhani mwanae ili awe mchungaji basi huanza kumwombea kipindi akiwa na mkubwa, au kama ni raisi wa nchi mzazi huanza kumwombea mwanae kipindi cha kampeni kuanza. Shetani yuko bize toka mimba ikiwa tumboni mwa mamayake, umesahau neno linasema walifundishwa uongo toka tumboni mwa mama zao

Hebu tuangalie mfano wa Yesu aliowafundisha wanafunzi wake,

v  Mathayo 13:24-19

“Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;
25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.
27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?
28 Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?
29 Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo”
.


Huu ni mfano wa Yesu juu ya shamba la ngano na mkulima wa shamba hilo. Mkulima alipomaliza kupanda zile ngano akaondoka zake kurudi nyumbani. Usiku walipokuwa wamelala adui yake alikuja akapandikiza na yeye mbegu za magugu katika shamba lile lile. Huyu mkulima pamoja na kuwa na watumwa hakuwaweka walinde au yamkini aliwaweka walinde lakini walilala usingizi. Ndio maana mstari wa 25 unasema “watu walipolala” ina maana na watumwa pia walilala usingizi na ulinzi haukuwa imara kiasi cha adui kupata muda wa kutosha kupandikiza mbegu zake za magugu. Walipotaka kuyang’oa yale magugu aliwakataza maana alihofu kung’oa hata mazao bora. Inanipa picha kuwa haya magugu yalikuwa sawa kabisa na ngano na isingekuwa rahisi kujua lipi ni gugu na ipi ni ngano, akawambia wasubiri mavuno.

Mkulima ni Mungu, shamba ni mwanao, mtumwa ni mzazi, mbegu ni kusudi la Mungu ndani ya mwanao na Magugu ni mapando ya shetani. Mpendwa shetani anakusubiri wewe mlinzi na mtumwa wa Mungu usinzie na ukisinzia anahakikisha amepanda roho yake ndani ya mwanao ambayo ikiendelea kukuwa hutaweza kutofautisha kati ya kusudi la Mungu na roho yake chafu, na mapando ya shetani yataenda yakikuwa pamoja na cha Mungu.


Ukimlinda mwanao akiwa tumboni tu au akiwa bado mdogo kisha ukaacha kulinda mambo yake ya ukubwani ikiwa ni pamoja na ndoa yake ujue umelala usingizi, mwovu atakuwahi atapanda magugu yake kwenye ndoa yake. Pia kama unamwombea mwanao tu umemwacha kumwombea mwenzi wake ujue shetani hatamgusa mwanao maana ana ulinzi wa ki Mungu atakimbilia upande wa pili wa mwenzi wake atapanda magugu yake, kipindi ambacho mwanao anaoana na huyu tayari kutakuwa na magugu yatachanganyikana na mbegu. Haijalishi unamfahamu mwenzi wa mwanao au humfahamu isikusumbue, ili mradi Mungu amekwambia mwanao sio Mtawa, ina maana ataoa au kuolewa, kwa hili inamaanaisha kuwa tayari yuko mumewe au mkewe. Biblia inasema Eva alitoka ubavuni mwa Adamu (Mwanzo 2:21) kama mwanao ni msichana ujue yupo Adamu wake kadhalika kama ni Adamu ujue yupo Eva wake. Wewe mwombee naye ili shetani asije kupanda magugu ndani yake. Huwa wazazi wengi wanawapinga watoto wao wasiolewe au kuoa kijana fulani na wanatoa kila aina ya sababu. Ukiwauliza waliwahi kumwombea mwenzi wa mtoto wao? Wanajibu tulimwomba Mungu ampe wa kufanana naye. Mungu anakuwa ameshamweka wa kufanana naye, suala linakuja, je ulimlinda ibilisi asiweke vya kwake ndani yake? Maana kwa habari ya kufanana Mungu alikwisha kamilisha kuumba kilibaki wewe kumlinda. Wewe ukipata neema ya kulijua neno la Kristo lifanyie kazi maana hujui kama mzazi (mzazimwenza) wa huyo mwenzi wa mwanao anajua kumlinda mwanae au la. Wewe linda wote ibilisi asipate kupanda magugu yake. Usipolinda usishangae mwanao kukuletea mwislamu kuwa anataka kuona naye, magugu yanakuwa yamepandwa ndani yake hapo ndipo ugomvi na mwanao huanza,

Hebu tuangalie kwa mfano wa mtoto ambaye ni Mchungaji au mtume, nabii, mwinjilisti au mwalimu. Shetani hujitahidi kupanda roho ya upinzani ndani ya mtoto anakuwa ni mpinzani wa neno la Mungu, na usishangae kuona anapenda mambo ya dunia kuliko neno la Mungu. Vita vyake vitakuwa ni kupinga kweli ya Mungu. Shetani hatamzuia asisome ila atamzuia asilijue neno la Mungu.

Mtoto ambaye ni kiongozi wa nchi kwa ngazi yoyote ile hata ya chini ya uenyekiti wa serikali ya mtaa, shetani atahakikisha huyu mtoto hapendi elimu, hata akisoma asifanikiwe. Funguka macho mzazi mjue mwanao ni nani kisha mpinge shetani asipande magugu yake. Kwani neno linasema

v  Efeso 4:27

“wala msimpe Ibilisi nafasi”.

“kangi mungampaga umohesi ubujo”(kinyakyusa)

“and do not give the devil a foothold(NIV)

Biblia ya kinyakyusa imetumia neno “ubujo” likiwa na maana makazi au makao, ikimaanisha usimpe shetani makao au makazi. Makao na makazi ni zaidi ya nafasi, ina maana usiruhusu shetani akapata mahali pa kukaa na kustarehe ndani ya mwanao. Na hii ya kiingereza imetumia neno “foothold”likiwa na maana nafasi inayomfanya mtu afanikiwe au endelee kufanikiwa sio nafasi ya kawaida hii ni nafasi ya kimafanikio. Paulo alikuwa anawambia wa efeso kuwa msijaribu kuruhusu shetani apate makao na makazi ndani yenu ambayo yatapelekea aendelee kufanikiwa ndani yenu.

Mzazi hakikisha kuwa unamlinda mwanao kiasi cha kwamba shetani asipate makao katika maisha yake.

    3. KILA MTOTO YUKO TOFAUTI NA MWENZIE NA WALA HAWAFANANI;

Kama ni mzazi mwenye watoto zaidi ya mmoja, kumbuka kuwa hao watoto hawafanani katika ulimwengu war oho, kila mmoja ana kusudi lake na kila mmoja anatakiwa kupitia njia yake katika ulimwengu wa roho, Japo katika mwili waweza kuwa wanafanana sana kitabia au maumbile. Kama mzazi usijaribu kuwafanyia vitu kijumla jumla, kila mmoja mfanyie kitofauti na mwenzie sawa na kusudi la kila mmoja. Sina maana uachilie roho ya utengano kati yao bali wawe na umoja lakini kila mtu aishe sawa na kusudi la Mungu ndani yake.

Hebu matzame mzee Yakobo alikuwa na watoto wa kiume 12, wakti wa kufa kwake kulipokaribia aliwabariki wanae wote. Hakuachilia Baraka kwa ujumla alimbariki kila mmoja peke yake kwa Baraka zake (Mwanzo 49:1-27) mfano alimwita Yuda alimpa fimbo ya enzi, Lawi na Simeioni kuwa watatawanyika, Dani atawawahukumu wenzie.

 Nataka tuone kuwa kila mtoto anatakiwa ahudumiwe kivyake vyake, kama ni maombi kila mmoja umweombee peke yake, usiwe na maombi ya kijumla. Ni hatari kuwaombea kijumla maana mwisho utakuta maombi yanamhusu mmoja tu na wengine hujawaombea. Mfano wewe ni mzazi wa Samsoni na Samsoni zisiwakumbe na samweli na Bwana amponye Samsoni, ujue hayo maombi yatakuwa ya Samweli peke yake japo umemtaja na Samsoni, kumbe Ungepaswa umwombee Samsoni Mungu amwongezee nguvu za kuwapiga wafilisti.

Msihi roho mtakatifu akufundishe kuwatofautisha watoto wako na akuwezeshe kila mmoja kumlea katika njia impasayo.waombee umoja kati yao ila usiwaombee kwa pamoja.


  4. KUSHINDWA KWA MWANAO NI KUSHINDWA KWAKO MZAZI

Mungu ameweka kusudi lake ndani ya mwanao. Wewe mzazi una jukumu la kuhakikisha hilo kusudi linakuwa na kumzalia Mungu matunda mema. Katika kuhakikisha hayo yanatendeka, chunga sana mzazi unaweka misingi gani ndani ya mwanao. Misingi uliyoiweka ndani ya mtoto ndio hiyo itamkuza mwanao, kama umeweka misingi ya sheani ndivyo hivyo hivyo mwanao atakuwa. Maana Mungu amekuamini wewe na kumpitisha huyo mtoto kwako na kukupa wewe dhamana ya kumtunzia katika mwili.

Wazazi wengi hujishau wakati wa utotoni hawawekei msingi ya Mungu watoto wao, wengi hudhani wakati mzuri wa kuweka misingi ya Mungu ndani ya watoto wao ni mpaka mtoto awe madarasa ya juu ya shule za msingi, au mapaka mtoto ajue kusoma na kuandika. Mpendwa unachelewa mtoto ni kama computa inahitaji kuwekewa program ili iweze kufanya kazi zake vema. Toka akiwa bado mchanga mfundishe habari za Mungu wako. Najua unashangaa kuwa akiwa mchanga ataelewa kweli, sikupi jibu kwanza mpaka ujijibu mwenyewe maswali haya. Je mtoto mchanga anaijuaje sauti ya mamake? Je amnamjuajae baba yake na kumtofautisha na wanaume wengine? Je anaielewaje lugha unayaomsemesha?

Umewahi kuwaza kwa kina je mtoto mwenye miaka saba (7) aweza kuwa mfalme juu ya taifa kubwa na kuliongoza vema katika Mapenzi ya Mungu. Soma habari za Yoashi (2falme11:21, 2falme 12:1-) akiwa na umri mdogo sana ambao kwa kizazi hiki angekuwa darasa la pili au tatu, aliweza kukaa chini ya kuhani Yehoyada akafundishwa mambo ya Mungu. Yoashi aliweza kutawala vizuri kuliko wafelme waliomtangulia waliokuwa na umri zaidi yake. Kilichomsaidia Yoashi kutawala vema sawa na Mapenzi ya Mungu ni ule msingi mzuri aliowekewa na kuhani. Mzazi weka msingi wa Mungu ndani ya mwanao angali bado ni mdogo, usijaribu kungoja akuwe ndipo uweke vya Mungu ndani yake, utakuwa umechelewa maana hakuna ubungo na moyo wa mwanadamu unaokuwa tupu, lazima uwe umejaza kitu ndani yake chaweza kuwa chema au kiovu, lakini bado utakuwa umejaza.

Tazama mtoto wa mpagani akizaliwa tu anapelekwa kuonyeshwa Mungu wa wazazi wake, hujawahi ona matambiko ya kumpokea mtoto mchanga? Wengine huwapeleka kwenye makaburi ya ndugu za mtoto waliokufa awali kisha wanainamishia kichwa cha mtoto juu ya kaburi. Wengine huwapeleka kwenye madhabahu za miungu yao kisha huwaacha huko walie mpaka sauti iwakwame. Yote haya ni kuhakikisha mtoto anakuwa na uhusiano an Miungu toka utoto wao.Au tazama watoto wa kiislamu, toka wadogo wanapelekwa kujifunza dini yao. Na walimu wanapewa kibali cha kuwapiga hata kama wataakufa haina shida ila lazima wamjue mungu wao. Wengine huwalipa hata walimu wa watoto wao ili wawafundishe watooto wao habari za Mungu wao. Yote haya ni kumjengea mtoto msingi ili akiwa mkubwa awe sawa na nenola mungu wa wazazi wake.

Msingi wa mwanao ni kitu muhimu sana. Ni mara ngapi umewafundisha wanao neno la Mungu, au hata kumlipa mwalimu wa kuja kuwafundisha nyumbani kwako. Mbona uanaweza kulipia twisheni (tution) ya masomo yao ya shule lakini hataki kulipia wajifunze neno la Mungu. Je umewanunulia vitabu vingapi  vya neno la Mungu na ukuwasimamia na kuwasaidia kuvisoma? Kumbuka

v  Yoeli 1: 3 inasema

Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine.”

v  Zaburi 78:3-4

Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia.
4 Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za Bwana, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya

Toka akiwa tumboni mwa mama msimulie mwanao matendo makuu ya Mungu aliyokutendea, endelea hata akizaliwa na ahata akiwa mzee, mfundishe matendo makuu ya Mungu. Usiache kuyatenda haya maana kwa ule wema wako na haki yako watoto wako hataacha kubarikiwa na Mungu baada yako.

v  Mithali 20:7

“Mwenye haki aendaye katika unyofu wake, Watoto wake wabarikiwa baada yake”

Kitendo chako cha kwenda katika njia nyofu za Mungu, wanao hubarikiwa. Kubarikiwa ni kuwa na utoshelevu katika mabo yote. Mzazi haitasaidia wanao kuwa na utoshelevu wa kila kitu mara baada yako kisha wakaikosa mbingu. Nakusihi kwa jina la Yesu, kazana pia kuwafundisha habari za Mungu, kama vile unavyoweka bidii katika masomo yao ya kawaida pia weka bidii katika neno la Mungu.


KUMBUKA

·     Kuwa mzazi unajukumu la kipekee kwa kila mtoto uliyenaye, kumwandalia mali za kurithi, kumwombea, kumfundisha njia za Mungu na hata kumwekea misingi imara ndani ya Mungu.

  • ·         Kila uongezapo mtoto au kila upatapo mtoto mwingine ujue unaongeza jukumu jingine jipya la kumlea huyo mtoto.

  • ·         Uzimlee mtoto kimazoea na kwa kumfananisha na wenzie.

  • ·         Tunza siri za Mungu akuambiazo juu ya mtoto wako. Jifunze kwa Rebeka.


No comments:

Post a Comment